WAHITIMU WA SHAHADA YA SAYANSI YA AFYA MAZINGIRA WAPIGWA MSASA
Posted on: October 26th, 2025NA WAF - DODOMA
Baraza la Wataalam wa Afya Mazingira limefanya semina elekezi kwa wahitimu wa Shahada ya Sayansi ya Afya Mazingira wanaotarajia kuanza mafunzo ya utarajali kwa mwaka wa mafunzo 2025/26.
Akizungumza leo Oktoba 25, 2025, katika semina hiyo Jijini Dodoma, Kaimu Msajili wa Baraza la Wataalam wa Afya Mazingira, Bw. Nashiri Mahiki, amesema wahitimu hao wanapaswa kufuata mwongozo wa usimamizi wa mafunzo ya watarajali wa Wizara ya Afya unaolenga kuboresha uratibu wa mafunzo na kusimamia kada ya Afya Mazingira.
Bw. Mahiki amesisitiza kuwa kila mhitimu anapaswa kuhakikisha katika kipindi cha mafunzo anafuata nidhamu, weledi na miiko ya taaluma.
Pia ameeleza kuwa mwongozo huo unaweka utaratibu wa usimamizi wa ngazi ya Wizara, Baraza, na vituo vya mafunzo, ikiwemo utoaji wa taarifa za maendeleo ya mafunzo kila robo mwaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza, Dkt. Hussein Mohamed amesema kwa mwaka wa mafunzo 2025/26, Baraza limepokea jumla ya maombi 157 ya wahitimu kutoka vyuo vya MUHAS, RUCU, SUZA, na baadhi ya vyuo vya nje ya nchi.
Wahitimu hao wamepangiwa vituo vya mafunzo katika mikoa 26 ya Tanzania Bara pamoja na vyuo vya Afya Mazingira.
Mafunzo hayo yataanza rasmi Novemba 2025 na kuhitimishwa Oktoba 2026.