Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI MCHENGERWA AKABIDHIWA OFISI NA MHE. JENISTA MHAGAMA.

Posted on: November 19th, 2025

Na WAF - Dodoma


Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Novemba 19, 2025 amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama.


Tukio la makabidhiano ya ofisi limefanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.


Waziri Mchengerwa amempongeza Mhe. Mhagama kwa utumishi wake hodari katika Wizara mbalimbali nchiini ikiwemo Wizara ya Afya ambapo amefanya kazi kubwa ya kuboresha Sekta hiyo na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.


“Mhe. Rais ameahidi ndani ya siku 100 atafanya mageuzi makubwa ya Sekta ya Afya nchini, nashukuru kwa hatua nzuri ambayo ulishaanza utekelezaji wake ikiwemo suala la Bima ya Afya kwa wote pamoja na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza nchini ambayo yanaleta athari kubwa ndani ya jamii” amesema Waziri Mchengerwa.


Mhe. Mchengerwa amemtakia kila la heri Mhe. Mhagama na kuahidi kuendelea kushirikiana. Amesema kuwa Wizara ya Afya ni mhimili mkubwa sana katika usalama wa nchi hivyo watajitahidi kuhakikisha ndoto za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinatimia kwa kutekeleza kikamilifu yale yote yaliyomo kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.


Awali akizunguma, Mhe. Mhagama amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kuongoza Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Afya katika kipindi chote cha muhula wa kwanza wa Serikali ya awamu ya Sita.


Mhe. Mhagama amewapongeza Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Mhe. Dkt. Frolence Samizi kuwa Naibu Waziri wa Afya huku akiwaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maendeleo ya Sekta ya Afya ili kuzimiza maono ya Mhe. Rais ya uboreshaji wa huduma za afya nchini.