Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YAENDELEA KUJIZATITI UTOAJI ELIMU YA AFYA KWA UMMA, YAPOKEA VIFAA VYA M.84

Posted on: February 18th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Afya imepokea vifaa vya matangazo ya elimu ya afya kwa umma kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) vyenye thamani ya shilingi Milioni 84,870,000/= kwa lengo la kurahisisha utolewaji wa elimu ya afya kwa umma. 


Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amepokea vifaa hivyo leo Februari 18, 2026 kwa niaba ya Serikali katika ofisi za Wizara ya Afya zilizopo mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma. 


"Vifaa hivi vinatolewa kwa mikoa mitatu ya Kigoma, Dodoma pamoja na Mwanza ambavyo seti yake ni pamoja na TV, betri, computer, spika, laptop, printer, invetor, microphone na connector wire. 


Aidha, Dkt. Magembe amesema vifaa hivyo vitasaidia katika utoaji wa elimu kwa wananchi kwa lengo la kuzuia magonjwa kwa kuwa wananchi wakipata elimu wanauwezo wa kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo ya milipuko. 


"Vifaa hivi pia tutavitumia tena kwenye ngazi ya jamii, kwa sababu katika maeneo ambayo tulifanya vizuri ni kuwaelimisha kina mama juu ya umuhimu wa kwenda mapema kwenye kituo cha huduma anapokuwa mjamzito, umuhimu wa kutoa chanjo kwa watoto, jambo ambalo kimechangia kuounguza vifo vitokanavyo na uzazi na vile vya watoto chini ya miaka mitano amesema Dkt. Magembe.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Ona Machangu amesema wameanza kufunga vifaa hivyo kwenye magari ambayo yanaweza kupaki sokoni au stendi kwa lengo la kutoa elimu. 


"Lakini tumetengewa fedha kwa ajili ya kununuliwa gari maalumu ambalo kazi yake itakua ni kupita barabarani pamoja na sehemu mbalimbali za mikusanyiko ya watu ili kutoa elimu ya afya kwa wananchi," amesema Dkt. Machangu.