WANANCHI WAHIMIZWA KUTUMIA HUDUMA ZA AFYA KWA NGAZI SAHIHI ZA MATIBABU – DKT. SAMIZI
Posted on: February 20th, 2026Na Shaban Juma, WAF-Kilimanjaro
Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kuweka mazingira wezeshi ya utoaji huduma kuanzia ngazi ya msingi, Wilaya, hospitali za rufaa za mikoa, rufaa za kanda hadi Taifa, akiwataka wananchi kufuata utaratibu kulingana na aina ya huduma.
Dkt. Samizi ametoa kauli hiyo leo Februari 20, 2026 mara baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo, ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya Mabogini–Chekereni–Kahe, ambapo akijibu swali la mwananchi lililohusu upatikanaji wa huduma za afya.
Amesema maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita yameongeza uwezo wa vituo vya afya na hospitali za wilaya kutoa huduma ambazo hapo awali zilipatikana katika hospitali za rufaa pekee.
Aidha, Dkt. Samizi amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya ngazi za matibabu yatawawezesha wananchi kupata huduma kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa ubora unaostahili.
Pia, amewahimiza wananchi kujiunga na mifumo ya bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuchangia uendelevu wa maboresho yanayoendelea kutekelezwa na Serikali.