SADC YAWEKA MSINGI WA PAMOJA WA UNUNUZI WA BIDHAA ZA AFYA
Posted on: February 21st, 2026Na Shaban Juma, WAF – Johannesburg
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia Mkutano wa Makatibu Wakuu na Wataalam wa Afya imejadili mpango wa kuanza utekelezaji wa ununuzi wa pamoja wa dawa na bidhaa za afya (SADC Pooled Procurement Services – SPPS) hatua ambayo itaimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya nchini Tanzania
Ujumbe wa wataalam kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Daud Tayari, leo februari 22, 2026 Nchini Afrika Kusini ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Afya na Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya UKIMWI.
Tanzania imeeleza matarajio yake ya kutumia mpango wa SPPS kama nyenzo ya kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya, siyo tu kwa mahitaji ya Tanzania bali pia kwa nchi nyingine za ukanda wa SADC, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa upatikanaji wa bidhaa za afya na kukuza uchumi wa kikanda.
Mkutano huo umejikita kujadili kuanza kwa utekelezaji wa huduma ya ununuzi wa pamoja wa dawa na bidhaa za afya kwa nchi wanachama wa SADC, maarufu kama SADC Pooled Procurement Services (SPPS), unaoongozwa na Medical Stores Department (MSD) kutoka Tanzania.
Katika mkutano huo wa ngazi ya wataalam na makatibu wakuu, wajumbe wamejadili hatua muhimu ya kurahisisha rasimu ya katiba (draft charter) itakayounda taasisi ya SPPS kwa kuzingatia kanuni ya subsidiarity, ikiwa ni maandalizi ya uamuzi wa mwisho unaotarajiwa kufanywa na Mawaziri katika mkutano wao.
Aidha, mkutano umejadili mpango wa nchi wanachama kuanza ununuzi wa pamoja kwa kutumia mfumo wa unununzi wa kikundi (group contracting), unaolenga kuongeza ufanisi wa manunuzi, kupunguza gharama za bidhaa za afya, na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika ukanda wa SADC.