SERIKALI, WHO YAENDELEZA AFUA KUDHIBITI MAGONJWA YATOKANAYO NA MAJI
Posted on: February 19th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF- Morogoro
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani (WHO) imetoa mafunzo kwa Wataalamu wa afya ya mazingira na wa vituo vya afya mipakani kuimarisha usalama wa maji ili kuilinda jamii dhidi ya magonjwa ya kuhara, kutapika, homa ya matumbo (typhoid) na kuhara damu.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo leo Februari 19, 2026 mkoani Morogoro, Bw. Shikabwe Msafiri amesema lengo ni kuwajengea uwezo wataalamu hao waweze kupima na kufuatilia ubora wa maji.
“Wataalamu wameweza kufahamu namna sahihi ya kupima ubora wa maji kwa kutumia kifaa kinachoitwa 'DelAgua Kit', ambacho hutumika kutambua kama maji ni salama au yana vimelea hatarishi vinavyoweza kusababisha magonjwa,” amesema Bw. Msafiri.
Aidha, ameongeza kuwa ni jukumu la wataalamu wa afya ya mazingira na wa mipakani kutambua usalama wa vyanzo vya maji na kuchukua hatua stahiki kulinda afya ya jamii, pamoja na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya maji salama majumbani.
“Wananchi wanatumia maji kutoka vyanzo mbalimbali kama visima, mabomba, mito na maziwa kwa matumizi ya kupika, kunywa, kuoga na kuosha vyombo. Maji salama si ya kunywa tu, bali hata kwa kunawa mikono au kuoga tunahitaji kutumia maji yaliyo salama,” amesisitiza Bw. Msafiri.
Kwa upande wake, Afisa Afya wa jiji la Tanga na Mkuu wa Kitengo cha Afya ya Kinga, Bw. Lwitiko Malabeja, amesema mafunzo hayo yamewawezesha washiriki kutambua namna bora ya kuchukua sampuli za maji, kutumia kifaa cha kupimia ubora wa maji pamoja na kubaini changamoto zilizopo katika vyanzo vya maji.
“Kupitia kifaa hiki, sasa tunaweza kufanya vipimo vya sampuli kutoka katika vyanzo mbalimbali vya maji bila ya kwenda maabara na kutatua changamoto zitokanazo na matumizi ya maji yasiyo salama, hivyo kuilinda jamii dhidi ya magonjwa,” amesema Bw. Malabeja.