WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUBADILI MTINDO WA MAISHA KUEPUKA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Posted on: November 12th, 2025NA WAF – DODOMA
Watumishi wa umma wametakiwa kushirikiana katika kutoa elimu na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yanayosababishwa na mtindo mbaya wa maisha, ikiwemo ulaji usiofaa, matumizi ya vileo, na kutofanya mazoezi.
Wito huo umetolewa leo, tarehe 12 Novemba 2025 jijini Dodoma na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mama na Mtoto, Wizara ya Afya Dkt. Ahmed Makuwani, katika mafunzo maalum kwa Wakurugenzi na Watumishi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali kuhusu namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza mahali pa kazi.
Dkt. Makuwani amesema magonjwa kama presha, moyo, kisukari, kufeli kwa figo na mapafu ni hatari na yanaua watu wengi kuliko magonjwa ya kuambukiza kama Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu.
“Usipotambua mapema na kufanya vipimo, kubadilisha mtindo wa maisha, kutofanya mazoezi na kuzingatia lishe bora unaweza kujikuta kijana wa miaka 30 hadi 50 ukikabiliwa na matatizo yanayokuzuia kutimiza majukumu yako ya uzalishaji na kuingiza Serikali katika gharama kubwa za kukuhudumia kutokana na kupata magonjwa ambayo ungeweza kuzuia,” amesema Dkt. Makuwani.
Ameongeza kuwa “Zamani tulikuwa tunafanya mazoezi, tunalima, tunaendesha baiskeli, na kutembea. Sasa hatufanyi hivyo, na ndio sababu tumepata matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kasi. Tufanye mazoezi, tubadilishe mtindo wa maisha tunaoishi sasa na tuzingatie mwenendo bora wa vyakula vyetu,”.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa Yasiyoambukiza Dkt. Omary Ubuguyu amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu njia za kujikinga, kubadilisha mitindo isiyofaa ya maisha, na kushirikiana na watoa huduma za afya ili kupunguza athari za magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Ubuguyu amewataka viongozi hao kuendelea kutoa elimu ya afya kwa wananchi, kubadilisha mitindo isiyofaa ya maisha, na kuwahamasisha wananchi kuanza kwenda hospitalini kufanya vipimo ili kutambua dalili za mapema za magonjwa hayo.
Maadhimisho haya yanafanyika kuanzia tarehe 10 hadi 15 Novemba 2025, yakiwa na kauli mbiu isemayo: “Chukua Hatua Sasa Kudhibiti