Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

IMARISHENI UDHIBITI WA MATUMIZI YA FEDHA ZA GLOBAL FUND- DKT. SHEKALAGHE

Posted on: November 12th, 2025

Na. WAF, Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amewataka watekelezaji wa mradi wa afua za UKIMWI na Kifua Kikuu ngazi ya jamii kuimarisha udhibiti wa matumizi sahihi ya fedha za kutekelezea mradi huo.

Dkt. Shekalaghe ameyasema hayo Novemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha uzinduzi wa utekelezaji wa afua za UKIMWI na Kifua Kikuu ngazi ya jamii mzunguko wa saba (7), mradi unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia ( Global Fund).

Amesema ni muhimu kuhakikisha mifumo ya kifedha ya mradi inaimarishwa na kutumika vizuri kwa uadilifu na kuzingatia taratibu zote zilizowekwa na kwa wakati.

“Mtekelezaji wa mradi huu kwa mzunguko wa saba, namba mbili ni Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC) pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, mradi unatarajiwa kukamilika mwakani mwezi Disemba, hivyo niwasisitize watekelezaji wa mradi kila shilingi ambayo inapatikana kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu ikatumike vizuri na kufuata taratibu zilizowekwa,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Amewataka pia kuhakikisha malengo yaliyowekwa kwenye magonjwa ya UKIMWI na Kifua Kikuu yanafikiwa kwa wakati uliopangwa.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema kumekuwa na mafanikio makubwa ya mradi huo kwa awamu zilizopita, maambukizi ya VVU yamepungua kwa asilimia 61, kutoka wagonjwa takribani 110,000 mwaka 2010 na kufikia 43,000 mwaka 2024 na kwa upande wa Kifua Kikuu kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi kufikia 172 kwa kila watu 100,000 mwaka 2024.

“Kinachokwenda kufanyika ni kuendelea kupunguza zaidi kwa kuanza kujikita katika makundi yaliyo kwenye hatari zaidi kama vijana walio kwenye umri wa kuzaa na kufika ngazi ya jamii kwa kuibua watu wenye dalili za Kifua Kikuu na walio kwenye mazingira hatarishi ya kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kuhakikisha wako kwenye dawa. Afua za tiba, kinga na za elimu tunakwenda kuziwekea mkazo zaidi,” amesema Dkt. Magembe.