ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 4 KUJENGA SHULE YA TABIBU KWA KUTEKELEZA AGIZO LA MAKAMU WA RAIS
Posted on: October 22nd, 2025
Na WAF - Arusha
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya tabibu itakatojengwa wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ili kuzalisha wataalam bobezi katika sekta ya afya watakaotoa huduma bora za afya nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe amesema hayo Oktoba 21, 2025 wakati wa makabidhiano ya hati ya umiliki wa eneo la ujenzi wa shule hiyo katika Halmashauri ya Rombo, yaliyofanyika katika Kituo cha Maendeleo ya Elimu katika Afya (CEDHA) kilichopo Jijini Arusha.
"Serikali imetoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo itakayohudumia wananchi wa eneo hilo pamoja na utoaji wa elimu ya afya ikiwa ni maelekezo na ahadi ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango aliyoitoa alipofika wilayani humo kwa ajili ya ufunguzi wa hospitali ya wilaya," amesema Dkt. Shekalaghe.
Aidha, Dkt. Shekalaghe amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza mchakato wa manunuzi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho kitakacho wahudumia wanachi na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda kwa kutimiza wajibu wake kuhakikisha chuo hicho kinamalizika haraka na kuanza kutoa mafunzo.
"Nitoe rai kwa wananchi kuhakikisha wanatumia fursa ya chuo hicho kitakapomalizika kujengwa kwa kuwapeleka watoto kupata elimu pamoja na kulinda miundombinu itakayokuwepo ili tuendelee kufaidika na chuo hiki," amesema Dkt. Shekalaghe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya, Dkt. Saitore Laizer amesema tasnia ya mafunzo ya sekta ya afya nchini imepata historia nyingine kutokana na ujenzi wa chuo hicho kitakachotoa programu zaidi ya tano (5) zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 2,000.
Naye, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Dkt. Deogratius Maruba amesema makabidhiano ya hati hiyo ya kiwanja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo cha afya wilayani humo ni fursa kwa wananchi wa Rombo.
Amesema ujenzi wa chuo hicho utawezesha shughuli za uchumi wilayani humo kuongezeka kwa kuuza bidhaa ikiwemo wataalam watakaozalishwa chuoni hapo ambao watatoa huduma kwa jamii.