Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WAONDOA UVIMBE ULIODUMU KWA MIAKA TISA

Posted on: October 23rd, 2025

Na. WAF, Kwimba-Mwanza

Madaktari Bingwa wa Rais Samia wamefanya upasuaji wa uvimbe shingoni (Goita) kwa Bi. Bernadetha Makoye uliomtesa kwa zaidi ya miaka tisa(9).

Upasuaji huo umefanyika Oktoba 22, 2025 katika hospitali ya wilaya ya Kwimba wakati kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia ikiendelea mkoani Mwanza.

Akieleza mara baada ya upasuaji Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Mwinyimkuu Lesso amesema upasuaji ulifanyika vizuri kwa ushirikiano mkubwa na timu ya wataalam wa hospitali hiyo ambao mara kwa mara wamekuwa wakijengewa uwezo.

“ Kazi ilikuwa ni rahisi kutokana na ushirikiano na maelekezo tuliyokuwa tunapeana na wataalam wenzangu, lakini pia kupitia kambi hizo wataalam walioko kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wamekuwa wakipata mafunzo ambayo yamekuwa yakisaidia tunaporudi kwa mara nyingine hivyo kwa pamoja tunafikia lengo la kuwahudumia Watanzania,” amesema Dkt. Lesso

Ameongeza kuwa kwa sasa mgonjwa anaendelea vizuri na amekwisha amka na kwamba kambi hizo zina umuhimu mkubwa kwakuwa zinawapatia huduma za kibingwa wananchi kwa gharama ndogo za kituo husika na kumuondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma,” ameongeza Dkt. Lesso

Kwa upande wake Bi. Bernadetha Makoye amesema uvimbe huo ulikuwa unamkosesha furaha na amani na wakati mwingine kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake.

“Ninaishukuru Serikali kwa kuendelea kutuletea hawa madaktari bingwa katika hospitali zetu za wilaya jambo linalotusaidia kupata huduma karibu na maeneo yetu hivyo kupunguza gharama maana hapa nilitakiwa kwenda Hospitali ya Bungando lakini nimefanikiwa kutibiwa hapa hapa nyumbani,” amesema Bi. Bernadetha.