SERIKALI YA TANZANIA YAENDELEA KUSHIRIKIANA NA GFF KWA KUTAMBUA MCHANGO WAO
Posted on: May 20th, 2025
Na WAF - Geneva, Uswisi
Waziri wa Afya Tanzania Mhe. Jenista Mhagama akiambatana na Waziri wa Afya (Zanzibar) Mhe. Nasoro Mazrui leo Mei 20, 2025 wamekutana na uongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Ufadhili kwa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto (GFF) na kueleza mafanikio ya ushirikiano wao.
Waziri Mhagama katika kikao hicho kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 78 wa Shirika la Afya Duniani (WHO), amesema miongoni ma mafanikio waliyoyapata kutokana na ushirikiano huo ni pamoja na msaada wa thamani ya Dola za Marekani Milioni 40 zilizosambazwa katika mikoa tisa (9).
"Ushirikiano kati ya GFF na Tanzania umekuwa na mchango mkubwa nchini kwetu katika kubadilisha sekta ya afya, uratibu wa karibu, msaada kifedha na mwitikio kutoka GFF ni wa kipekee na umetuwezesha kukabiliana na changamoto za afya kwa haraka," amesema Waziri Mhagama.
Aidha Waziri Mhagama ameomba GFF kuendelea kushirikiana na Tanzania hasa kwa msaada wa kifedha na kiufundi ili kuendelea kuiwezesha Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika kuboresha afya na ustawi wa wananchi wote.
"Lakini pia tunaomba GFF iangalie uwezekano wa kuiwezesha Tanzania kuchangia kwa pamoja (core finance) katika programu mpya ya Benki ya Dunia inayotarajiwa (Sustainable Health Innovations for Future Transformation - SHIFT)," amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameushukuru uongozi wa GFF kwa uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na GFF.