Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAKIDHI MATAKWA YA WANANCHI

Posted on: May 22nd, 2025

Na WAF - NKASI, RUKWA


Wanufaika wa huduma za Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia Wilayani Nkasi wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa  kukidhi matakwa  ya wananchi katika utoaji wa huduma mbalimbali za afya.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mei 22, 2025 Katika Hospitali ya Wilaya ya Nkasi ilipowekwa kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia, wakazi hao wamesema kuwa ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya afya ni mkubwa jambo lilichochochea kijitokeza kwa wingi kuhudhuria kambi hiyo kwani imezingatia mahitaji yao.


“Nilivyosikia sifa zao kwa kweli mimi mwenyewe nilihamasika sana kwakuwa nlikuwa natamani na mimi siku moja  nitibiwe na madaktari bingwa,” amesema Bi. Esther Mvuna mkazi wa kitongoji cha Msukumilo ambaye ni mnufaika wa huduma za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia. 


Licha ya huduma bora zinazoendelea kutolewa wanufaika pia wamepongeza utaratibu uliotumika kuhakikisha kila mmoja anafikiwa na taarifa za ujio wa Mabingwa hao


“Kwanza tunawashukuru viongozi wetu wa mitaa na madaraja mbalimbali wa wilaya hii wamefanya wawezavyo ili kila mwananchi aweze kuifikia hii huduma, ndiyo maana mmeona hata muitikio mkubwa,” amesema  Bw. Sharifu Kisi mkazi wa kata ya Sintali ambaye ni mnufaika wa huduma za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia.


Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi Dkt. Thomasi Ndeule amesema muitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kutokana na jinsi walivyoitangaza kambi hiyo.


“Tunamshukuru Mhe. Rais na Serikali yake sikivu ambayo imegusa na kutoa huduma kwa jamii kulinga na matakwa yao kwakuwa kama wangeikosa  huduma hiyo hapa ingewalazimu kuifuata Mbeya hospitali ya kanda,” amesema Dkt. Ndeule.