TANZANIA YAENDELEA KUWA KINARA DUNIANI KWENYE MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI
Posted on: May 21st, 2025
Na WAF - Geneva, Uswisi
Zaidi ya akina mama na watoto 150,740 waliokuwa na dharura ya huduma ya uzazi wamepata huduma ya usafiri wa haraka kupitia mfumo wa rufaa ngazi ya jamii (m-mama) hadi kufikia Mei, 2025 na kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wachanga wapatao 6,279.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Mei 21, 2025 kwenye kikao cha pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wenye lengo la kujadili namna ambavyo nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya mbali zimetumia mikakati mablimbali ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ikiwemo ujenzi wa miundombinu, matumizi ya teknolojia, wahudumu ngazi ya jamii na mafunzo ya watumishi.
Katika kikao hicho, Mganga Mkuu wa Serikali ameelezea namna Serikali ilivyowekeza katika kuboresha miundombinu ya afya hasa ngazi ya msingi ikiwemo majengo, vifaa na vifaa tiba na kuongeza vituo vinavyotoa huduma za Afya vyenye huduma za dharura za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.
"Pamoja na ujenzi wa miundombinu, bado tuliona kuna wajawazito ambao wanapopata dharura wanahitaji kusafirishwa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine chenye huduma za ubingwa ili kupata huduma hizo na ndipo safari yetu ya M-Mama ilipoanza," amesema Dkt. Magembe.
Amesema, huduma ya m-mama imeipatia nchi uzoefu na iko tayari kushirikiana na jamii za Kimataifa ili kwa pamoja kupata suluhisho bunifu na za kiteknolojia kwa usafiri wa dharura ambao unaweza kuwa nafuu na endelevu katika maeneo ya pembezoni na yasiyofikika kirahisi.
Uzoefu wa Tanzania katika utoaji wa huduma za usafiri wa *m-mama* ni ubunifu unaoshirikisha Sekta ya Umma, binafsi na Jamii katika kuboresha huduma za dharura kwa kuangalia mazingira na kutumia rasilimali zilizopo eneo husika
Dkt. Magembe amesisitiza kuwa Tanzania iko tayari kupata uzoefu wa Jumuiya ya Kimataifa ili kufanya vifo vya mama na watoto wachanga kuwa historia kuelekea mwisho wa utekelezaji wa malengo ya kidunia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikika chini ya 70 Kwa kila vizazo hai 100,000 kufikia mwaka 2030.