Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

RC MBEYA AWATAKA WANAUME KUTOWAKIMBIA WAKE ZAO KWASABABU YA FISTULA

Posted on: May 23rd, 2025

Na WAF - Mbeya


Wanaume wametakiwa kuishi ahadi na kiapo cha ndoa na kuacha kuwanyanyapaa wanawake wakati wanapopata ugonjwa wa fistula na badala yake wasaidie kuwatafutia matibabu kwasababu ugonjwa huo unatibika kabisa tena bila malipo. 


Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt. Juma Zuberi Homera wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani leo tarehe 23, Mei, 2025 Jijini Mbeya.


"Kiapo cha ndoa kinasema mtaishi wote kwa shida na raha, inapotokea mmoja anapoumwa uwe mke au mume inatakiwa muwe pamoja mpaka kifo kitakapowatenganisha hapa tusikimbie majukumu tuwatie moyo wenye changamoto ili tuweze kuishi nao vizuri," amesema Dkt. Omera.


Dkt. Omera amesema kuwa nchini Tanzania takwimu zinaonesha kati ya wanawake 2,500 hadi 3000 wanapata ugonjwa wa Fistula na kati yao 1,500 ndio wanabahatika kupatiwa matibabu, akibainisha kuwa fistula bado ni changamoto katika jamii kwani wagonjwa wengi hawawi wazi kutokana na suala la unyanyapaa.


"Ujauzito ni jambo la heshima sana na mtoto ni tunu, mama anapokuwa mjamzito matarajio yake na shauku ni kujifungua mtoto akiwa salama, mwenye afya njema na yeye pia akibaki salama tayari kwa kazi ya ulezi, tatizo lolote wakati wa kujifungua ni pamoja na fistula, inamletea majonzi na hata msongo wa mawazo na kushindwa majukumu yake", aliongeza kiongozi huyo wa Mkoa.


Naye Shuhuda wa tiba ya Fistula Bi. Atuganile Mwambuli wakati akipokea faraja ya Mkuu wa mkoa wodini katika Hospitali ya Kanda Mbeya alisema alitengwa na familia pamoja na mume wake hivyo matibabu haya ni faraja kubwa kwake.   


"Ndugu walinitenga kwa ajili ya hali yangu sasa kama ndugu wanakutenga je?,  mme wako atakubali kukaa na wewe, nashukuru Rais Samia na Mashirika yayowezesha kupatikana kwa tiba hii inayotolewa bure, anamilizia kwa kusema Bi. Atuganile Mwambuli.


Shuhuda huyo aliongeza kuwa hata baadhi ya wagonjwa wenzake kabla ya kufanyiwa upasuaji na tiba walikuwa wanashindwa hata kutoka nje kwa kuwa walishindwa kudhibiti mkojo na kuwekela wa wengine lakini baada ya tiba wanalala vizuri bila kuona ata tone la mkojo kitandani.


Mratibu wa afua za Fistula Tanzania Bi. Fidea Obimbo ameitaja Mikoa inayoongoza kwa changamoto ya Fistula kuwa  ni pamoja  na Dar es Salaam, Mwanza, Mara na Kagera akiitaja mikoa ya kanda ya ziwa kuwa na idadi kubwa ya uzazi.


Wizara ya Afya kwa kushikiriana na wadau wa maendeleo, imeendelea kusimamia huduma bora za afya ya mama na mtoto, ikiwemo kuboresha huduma za upasuaji wa dharura, ufuatiliaji wa kina wa ujauzito na utoaji elimu kwa umma kuhusu uzazi salama.