WIZARA YA AFYA YAWEKA MKAZO KUIMARISHA HUDUMA RAFIKI KWA VIJANA BALEHE
Posted on: September 29th, 2026Wizara ya Afya kupitia Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali UNFPA , Ubalozi wa Uswiss,Doris Mollel Foundation, MSI,Pathfinder na UMATI inaendelea kuimarisha uwezo wa watoa huduma za afya katika utoaji wa huduma bora, jumuishi na rafiki kwa vijana na na vijana balehe ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha afya na ustawi wa kundi hilo nchini.
Akizungumza leo Septemba 29,2026 Jijini Dar es salaam, Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa Vijana kutoka Wizara ya Afya, Gerald Kihwele, wakati akiwasilisha mada katika Jukwaa la Kitaifa la Afya ya Uzazi na Jinsia kwa Vijana na Vijana Balehe, amesema kuwa mafunzo kwa vitendo (Apprenticeship) ni muhimu katika kujenga umahiri wa watoa huduma za afya, kukuza viwango vya utoaji wa huduma rafiki kwa vijana na balehe, pamoja na kuimarisha usimamizi shirikishi na ujifunzaji endelevu.
Ameeleza kuwa, kupitia mafunzo hayo watoa huduma huimarisha ujuzi wa mawasiliano, uzingatiaji wa usiri wa taarifa za wateja na utekelezaji wa afua za kuboresha ubora wa huduma katika vituo vya afya.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ujumuishaji wa huduma za Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Balehe (RMNCAH) pamoja na huduma za Afya ya Uzazi na Jinsia (SRHR), kuongeza ushiriki wa wanaume na vijana katika huduma hizo, pamoja na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathmini na uwajibikaji.
Katika kuhitimisha Dkt. Kihwele ameeleza katika hatua zinazofuata, imependekezwa kuendelea kusambaza miongozo katika ngazi zote, kuimarisha uelekezi na usimamizi shirikishi wa watoa huduma, pamoja na kuendeleza ushauri elekezi na utetezi ili kuhakikisha uendelevu wa huduma bora, jumuishi na zenye heshima kwa vijana na Vijana balehe nchini.