Ministry of Health

MUHIMBILI YAWEKEZA TSH.BILIONI 1.63 KUHAKIKISHA UPATIKANAJI ENDELEVU WA HEWA TIBA

Posted on: September 30th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF–Dar es Salaam

Hospitali ya Taifa Muhimbili imezindua Mtambo mpya wa Kuzalisha na Kusambaza hewa tiba wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 1.63, ukiwa na lengo la kuhakikisha upatikanaji endelevu wa hewa tiba kwa wagonjwa katika majengo mbalimbali ya hospitali hiyo.

Akizungumza leo Septemba 30, 2026 wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema uwekezaji huo unalenga kutoa suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba iliyokuwa ikijitokeza katika hospitali hiyo kutokana na uchakavu wa miundombinu na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma.

Amesema upatikanaji wa hewa tiba ni sehemu muhimu ya huduma kwa wagonjwa mahututi na wa dharura, hivyo mfumo wake unapaswa kuwa wa uhakika na endelevu wakati wote.

“Leo hatubadilishi mtambo tu, tunabadilisha mfumo,” amesema Waziri Mchengerwa.

Waziri amesema mradi huo unatarajiwa kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika upatikanaji wa hewa tiba na kuongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

“Hewa tiba ni dawa na dawa isiyopatikana kwa wakati si dawa tena; ni ahadi iliyovunjika,” amesema.

Amesisitiza kuwa uwekezaji huo hautakiwi kuishia katika uzinduzi wa mtambo, bali unatakiwa kuambatana na mfumo madhubuti wa matengenezo kinga ili kuhakikisha mtambo unaendelea kufanya kazi kwa ufanisi kwa muda mrefu.

Aidha, ameitaka Menejimenti ya Hospitali kuhakikisha mtambo huo unapunguza gharama za uendeshaji, unaongeza ufanisi wa huduma na kuondoa malalamiko ya ukosefu wa hewa tiba katika maeneo yanayohudumiwa na mfumo huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa ameelekeza kuwepo kwa ufuatiliaji wa takwimu za uzalishaji na matumizi ya hewa tiba pamoja na mwenendo wa malalamiko ya wagonjwa, ili kupima kwa vitendo matokeo ya uwekezaji huo.

Amesema takwimu zitakazokusanywa zitasaidia Serikali kutathmini ufanisi wa mradi na kuchukua hatua za kuhakikisha huduma ya hewa tiba inapatikana kwa wakati kwa wagonjwa wanaohitaji.