ILEJE DC YAIMARISHA UTAYARI KUKABILIANA NA UGONJWA WA EBOLA NA MVUA ZA EL NINO
Posted on: September 29th, 2026Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Mkoa wa Songwe, imeendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino, ikiwemo mafuriko na maporomoko ya ardhi, huku ikitenga Sh milioni 68 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya hatua za maandalizi.
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mazingira ya kijiografia ya Wilaya hiyo pamoja na kuwa eneo la mpakani a linalohusisha mwingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo Malawi .
Aidha, baadhi ya maeneo ya Ileje yana milima yenye udongo tifutifu, hali inayoweza kuongeza uwezekano wa maporomoko ya ardhi wakati wa mvua kubwa.
Akizungumza Septemba 29, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Bi Nuru Waziri Kidamba, amesema Halmashauri hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi mbalimbali kuhusu hatua za kujikinga na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na Ebola na El Nino.
Amebainisha pia maeneo yanayoweza kuathiriwa na maporomoko ya ardhi ni pamoja na Lubanda, Ngulilo, Luswisi, Sange na Ibada, huku maeneo ya Itumba, Chilete na Mbembe yakitajwa kuwa katika hatari ya kukumbwa na mafuriko,ameeleza kutokana na hali hiyo, Halmashauri imeendelea kuchukua hatua za maandalizi kulingana na mahitaji ya maeneo husika.
“Awali tulikuwa tumetenga Shilingi milioni tano, lakini baada ya maelekezo ya kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza, tulisitisha utekelezaji wa miradi mitatu na kukusanya Sh milioni 68 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya maandalizi,” amesema Kidamba.
Aidha, amesema Halmashauri imeomba takribani tani 25 za chakula kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), huku ikiwa na maghala maalumu kwa ajili ya uhifadhi wa chakula.
Hata hivyo amesema kuwa wananchi, wameendelea kuhamasishwa kutunza akiba ya chakula ili kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto zitakazoweza kujitokeza, amesisitiza zoezi la kuimarisha utayari linafanyika na Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya elimu ya Afya kwa Umma, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu–Sera, Uratibu na Bunge