MUHIMBILI YAWEKA MKAZO HUDUMA ZA KIBOBEZI KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO
Posted on: September 30th, 2026Na Andrea Kadege, WAF–Dar es Salaam
Hospitali ya Taifa Muhimbili imezindua Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto Tumboni (Maternal–Fetal Unit) pamoja na Chumba cha Kisasa cha Upasuaji wa Uzazi (Modular Theatre), hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kibobezi kwa wajawazito na watoto na kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.
Akizungumza leo Septemba 30, 2026,Jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema huduma hizo zinaiwezesha hospitali hiyo kuhama kutoka mfumo wa kusubiri changamoto zitokee na kuelekea katika utambuzi wa mapema wa vihatarishi na utoaji wa huduma kabla hali ya mgonjwa haijawa mbaya.
Amesema Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto Tumboni kitasaidia kuwafuatilia wajawazito mapema, kufanya uchunguzi wa kina wa vihatarishi kwa mama na mtoto, kutoa huduma stahiki na kuweka mpango wa kujifungua salama kulingana na mahitaji ya kila mama.
“Badala ya kumsubiri mama afike akiwa tayari katika hatari zitokanazo na ujauzito, sasa mama atafuatiliwa mapema, akiwa na mimba changa, kufanyiwa uchunguzi wa kina wa hatari kwake yeye na kwa mtoto.” amesema Mhe. Mchengerwa
Amesema hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali katika kutekeleza mkakati wa sifuri tatu katika kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga, hususan kwa kuimarisha huduma za kibobezi katika ngazi ya rufaa.
“Hospitali ya kisasa haipimwi kwa jinsi inavyopambana na dharura, bali kwa jinsi inavyozuia dharura zisitokee.” amesisitiza Waziri Mchengerwa
Aidha,amesisitiza kuwa, uwekezaji huo unatakiwa kuleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wagonjwa, ikiwemo kupunguza muda wa kusubiri upasuaji, kupunguza maambukizi na kuongeza usalama wa mama na mtoto wakati wa huduma.
“Kila mama atakayeletwa Muhimbili kwa changamoto za uzazi na kufanyiwa upasuaji, aondoke akiwa hai, yeye na mtoto wake,” amesema Waziri.
Amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya nchini, bado kuna umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika huduma za kibobezi kwa kuwa Muhimbili hupokea wagonjwa wa rufaa wenye changamoto kubwa zaidi za kiafya.