Ministry of Health

TANZANIA YAJIPANGA KUFADHILI NA KUPANUA AFYA KIDIJITALI

Posted on: September 30th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Kigali, Rwanda

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, amesema Tanzania imejenga msingi imara katika mabadiliko ya kidijitali kwenye sekta ya afya na sasa ipo tayari kushirikiana na wadau katika kufadhili, kupanua na kuendeleza mifumo iliyothibitisha uwezo wa kuboresha huduma za afya nchini.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Septemba 30, 2026 jijini Kigali, Rwanda, wakati akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika Mkutano wa Afrika wa Teknolojia za Afya 2026, ambako ameshiriki mjadala wa pamoja kuhusu namna ya kubadilisha mifumo ya afya iliyothibitisha mafanikio kuwa programu zinazoweza kufadhiliwa na kutekelezwa kwa kiwango kikubwa.

Amesema Tanzania, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha mabadiliko ya afya kidijitali kupitia Mikakati ya Taifa ya Afya Kidijitali na Mabadiliko ya Kidijitali, ikiwemo kuimarisha mifumo inayoweza kuwasiliana, usalama wa taarifa, ujuzi wa kidijitali na matumizi yanayowajibika ya akili mnemba.

Dkt. Samizi amesema Tanzania kupitia Mfumo Jumuishi wa Usanifu wa Teknolojia za Afya Tanzania, inalenga kuhakikisha uwekezaji katika teknolojia za afya unafanya kazi kama mfumo mmoja unaounganika, badala ya kuwa programu zinazojitegemea na kutengeneza mifumo iliyogawanyika.

Amesema hatua hiyo imewezesha maendeleo makubwa katika matumizi ya mifumo ya kidijitali katika vituo vya kutolea huduma, ambapo kumbukumbu za wagonjwa kwa njia ya kielektroniki zimefikia asilimia 100 katika hospitali za taifa, maalumu, rufaa za kanda na mikoa, karibu asilimia 99 katika Hospitali za Wilaya na zaidi ya asilimia 67 katika zahanati nchini.

Aidha, amesema Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya za Serikali (GoTHOMIS) sasa unaunganisha vituo 7,700 vya kutolea huduma za afya, ikiwemo zaidi ya zahanati 6,400 na karibu hospitali zote za Wilaya, huku mfumo wa m-mama ukiwa umewezesha kuratibu zaidi ya rufaa za dharura 214,000 za kina mama na watoto wachanga tangu mwaka 2021.