Ministry of Health

UHAMASISHAJI NA UTAYARI DHIDI YA EBOLA NA ATHARI ZA EL NINO WASHIKA KASI MKOA WA KILIMANJARO

Posted on: September 29th, 2026

Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu pamoja na wadau wa maendeleo UNICEF, Save the Children na Tanzania Interfaith Partnership (TIP), imeendelea na ziara ya uhamasishaji, ushirikishwaji wa jamii na tathmini ya utayari dhidi ya tishio la ugonjwa wa Ebola na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha.

Septemba 29, 2026 timu hiyo imefanya tathmini za utayari katika Mkoa wa Kilimanjaro Wilaya za Hai, Mwanga na Same kwa kushirikiana na viongozi na wataalamu wa afya katika ngazi za Mkoa na Halmashauri.

Aidha,Tathmini hiyo imelenga kupitia uwezo na utayari uliopo, kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa, pamoja na kuimarisha uratibu na mwitikio wa pamoja katika kukabiliana na maafa na milipuko ya magonjwa ikiwemo Ebola.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, kiongozi wa timu hiyo Mkoani Kilimanjaro Bi. Magdalena Dinawi amesema zoezi hilo la tathmini ni muhimu hususan katika kipindi hiki ambacho maeneo mbalimbali yanaendelea kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino.