Ministry of Health

KLINIKI YA HUDUMA ZA HARAKA KUBORESHA HUDUMA MUHIMBILI

Posted on: September 30th, 2026

Hospitali ya Taifa Muhimbili imezindua Kliniki ya Huduma za Haraka (Fast Track/VIP), inayolenga kutoa huduma zenye hadhi ya juu na kwa wakati huku mapato yatakayopatikana yakitumika pia kuboresha huduma kwa wananchi wasio na uwezo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Septemba 30, 2026, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa, amesema kliniki hiyo ni sehemu ya mikakati ya hospitali hiyo kuongeza vyanzo vya mapato na kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya Watanzania wenye uwezo wa kiuchumi.

Amesema baadhi ya Watanzania wenye uwezo wamekuwa wakisafiri nje ya nchi kutafuta huduma kwa kuhitaji faragha, heshima na huduma za haraka, hivyo kliniki hiyo inalenga kuweka huduma hizo ndani ya nchi.

Ameongeza kuwa kliniki hiyo itaendeshwa na wataalamu bobezi wa Muhimbili pamoja na wataalamu watakaoalikwa kutoka nje ya nchi, huku huduma zinazotolewa zikilenga kuwa na viwango vya juu.

Aidha, Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa mapato yatakayopatikana kupitia kliniki hiyo yataelekezwa katika kuboresha huduma kwa wagonjwa wasio na uwezo, kupitia mfumo wa ruzuku mtambuka ambapo malipo ya wenye uwezo yanachangia huduma kwa wananchi wenye mahitaji makubwa zaidi.

Waziri mchengerwa ameitaka Bodi ya Wadhamini kuhakikisha kliniki hiyo inaendeshwa kitaalamu, inajenga chapa imara na inatoa huduma bora, huku ikihakikisha ubunifu wa kuongeza mapato hauondoi wajibu wa Muhimbili wa kuwahudumia wananchi wasio na uwezo.