Ministry of Health

SERIKALI YASISITIZA UPATIKANAJI WA TAARIFA SAHIHI ZA AFYA NA HUDUMA RAFIKI KWA VIJANA

Posted on: September 30th, 2026

Na Mvuda Jaffer -WAF:Dar-es-Salaam

Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi za afya pamoja na huduma rafiki kwa vijana ikieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za afya ya uzazi na jinsia zinazowakabili vijana balehe nchini.

Akizungumza leo Septemba 30,2026 katika Jukwaa la Kitaifa la Vijana la Afya ya Uzazi na jinsia kwa Vijana Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Huduma za Watoto Wachanga na Vijana, Dkt. Felix Bundala amesema juhudi za kuboresha afya ya vijana hazipaswi kusubiri matatizo kujitokeza bali zinapaswa kujikita zaidi katika kinga na utoaji wa taarifa sahihi kwa wakati.

Dkt. Bundala amesema vijana wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya zikiwemo mimba za utotoni, maambukizi ya VVU, changamoto za afya ya akili, lishe na saratani zinazohusishwa na Virusi vya Papiloma ya Binadamu (HPV).

“Tunapofika kwenye kundi la vijana, mtazamo wetu lazima ubadilike. Hatuwezi kuangalia suala la survival pekee. Tunapaswa kuangalia namna ya kuwafanya vijana waishi maisha yenye afya,” amesema Dkt. Bundala.

Amesema changamoto si ukosefu wa taarifa pekee, bali pia namna taarifa hizo zinavyowafikia vijana na ubora wake, kwa kuwa vijana hutumia vyanzo mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii na intaneti. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha taarifa sahihi, zinazoeleweka na zinazokidhi mahitaji ya vijana zinapatikana katika majukwaa wanayoyatumia.

Aidha, Dkt. Bundala amesisitiza umuhimu wa kuunganisha juhudi za wadau wanaofanya kazi katika eneo la afya ya vijana, akieleza kuwa utekelezaji wa afua bila uratibu unaweza kusababisha huduma na taarifa kuwafikia vijana wachache kuliko ilivyokusudiwa.

Amesema mkakati wa miaka mitano unaoandaliwa unapaswa kuweka malengo na matokeo yanayopimika pamoja na kubainisha afua za kipaumbele zitakazowezesha kufikiwa kwa malengo hayo, Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kufikiwa katika mazingira yao mbalimbali, wakiwemo walio mashuleni na nje ya shule, katika familia, maeneo ya kazi, nyumba za ibada na mitandao ya kijamii.