Ministry of Health

WIZARA YA AFYA YASISITIZA UIMARISHWAJI WA UTAYARI WA KUKABILIANA NA DHARURA

Posted on: September 21st, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Dharura na Maafa, Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha mifumo ya afya, matumizi ya taarifa kwa wakati na uwezo wa timu za afya katika ngazi za mikoa na wilaya, ili kuwezesha utambuzi wa vihatarishi na uchukuaji wa hatua za mapema katika kukabiliana na dharura za afya.

Dkt. Erasto amesema hayo leo, Septemba 21, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha kutambulisha rasmi Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kujlandaa na Kukabiliana na Dharura (Health Resilience Programme) unaofadhiliwa na UK International Development.

Amesema pamoja na hatua zilizofikiwa katika kuimarisha mfumo wa afya nchini, bado kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha miundombinu, rasilimali watu, vifaa, dawa pamoja na mifumo ya taarifa inayowezesha mamlaka za afya kutambua vihatarishi mapema na kuchukua hatua stahiki, akisisitiza kuwa uwepo wa miundombinu pekee hautoshi bila kuwa na timu zenye uwezo na zinazofahamu majukumu yao wakati wa dharura.

“Tunahitaji kuwa na mifumo inayotuwezesha kufanya kazi kabla tatizo halijatokea au kuwa kubwa. Taarifa tunazopata kutoka katika jamii zinapaswa kutusaidia kuchukua hatua mapema na kujiandaa kabla hali haijawa mbaya,” amesema Dkt. Erasto.

Dkt. Erasto ameongeza kuwa taarifa zinazopatikana kutoka kwa jamii, familia, shule na vyanzo vingine zinapaswa kufikishwa kwa wakati katika mamlaka husika ili ziweze kuchambuliwa na kutumika katika kufanya maamuzi, huku akizitaka timu za afya katika ngazi za mikoa na wilaya kutumia taarifa hizo kutambua vihatarishi, kufanya maandalizi na kuchukua hatua kwa haraka kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao.