Ministry of Health

UTAYARI WA KUKABILIANA NA EBOLA WAPEWA KIPAUMBELE

Posted on: October 28th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua kujiandaa na kukabiliana na mlipuko wa Ebola, ikiwemo kuimarisha uchunguzi katika mipaka, uwezo wa upimaji wa maabara na ufuatiliaji wa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi.

Hatua hizo zimewasilishwa Oktoba 28, 2026, na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya kuhusu Ebola ulioitishwa na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) na kufanyika kwa njia ya mtandao, ukiwashirikisha viongozi wa afya, Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na washirika wa maendeleo.

Dkt. Samizi amesema hadi kufikia Oktoba 28, 2026, Tanzania haijathibitisha kisa cha Ebola nchini, lakini inaendelea kuimarisha utayari kutokana na mwingiliano na nchi zilizoathirika. Amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Dharura wa kukabiliana na Ebola aina ya Bundibugyo kupitia mfumo wa usimamizi wa matukio unaoshirikisha sekta mbalimbali na wadau.

Hatua zilizochukuliwa ni kuimarisha uchunguzi katika mipaka rasmi yote 59, kufuatilia tetesi na vifo visivyo vya kawaida, pamoja na kutoa Ushauri kwa Wasafiri Na. 18 wa Oktoba 17, 2026, unaowataka wasafiri kujaza dodoso la Afyamsafiri mtandaoni kuhusu safari na afya zao kabla ya kuingia nchini.

Aidha, Dkt. Samizi amesema Maabara ya Taifa ina uwezo wa kupima aina zote za virusi vya Ebola na kuchanganua vinasaba, huku maabara jongezi tatu zikiwa zimewekwa katika mikoa ya kimkakati na maeneo ya mipakani. Serikali pia imewafundisha wataalamu katika maeneo ya ufuatiliaji, upimaji, tiba, kinga dhidi ya maambukizi na maziko salama.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, amesema Tanzania imetuma tani 52 za dawa na vifaa kinga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na iko tayari kutuma wataalamu 12 wenye mafunzo maalumu kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko huo.