TANZANIA YAJIUNGA NA MPANGO WA WHO WA KUKOMESHA UNENE ULIOPITILIZA
Posted on: October 27th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF – Madrid, Spain
Tanzania imejiunga rasmi na Mpango wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa Kuharakisha Hatua za Kukomesha Unene Uliopitiliza (WHO Acceleration Plan to Stop Obesity), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha mapambano dhidi ya uzito uliozidi, unene uliopitiliza na magonjwa yasiyoambukiza yanayohusiana na ulaji.
Tangazo hilo limetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Unene Uliopitiliza (Global Obesity Summit) unaofanyika Madrid, Hispania, leo Oktoba 28, 2026.
Akizungumza katika mkutano huo, Prof. Sunguya amesema uamuzi huo unaonesha dhamira ya Tanzania ya kubadilisha maamuzi ya kisiasa kuwa hatua zinazoratibiwa, kupimika na zenye matokeo yanayoonekana, akisisitiza kuwa nchi iko tayari kuwajibika kwa washirika wa maendeleo na wananchi katika kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo ya afya.
Amesema takwimu za hivi karibuni za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria zinaonesha kuwa asilimia 36 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 nchini wana uzito uliozidi au unene uliopitiliza, huku asilimia nne ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakiwa na hali hiyo. Ameeleza kuwa changamoto hiyo inaenda sambamba na utapiamlo, ambapo asilimia 30 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 12 wana uzito pungufu na asilimia tatu wanakabiliwa na ukondefu unaotokana na utapiamlo.
Prof. Sunguya amesema hali hiyo inaonesha kuwa utapiamlo unaotokana na upungufu wa lishe na ule unaohusishwa na uzito uliozidi unaweza kuwepo katika jamii moja na hata kaya moja, hivyo kuhitaji hatua zinazozingatia ushahidi wa kisayansi, tofauti za kijamii na kiuchumi pamoja na mahitaji ya makundi mbalimbali, hususan watoto na wanawake walio katika umri wa kuzaa.
Ameeleza kuwa Tanzania tayari imepiga hatua katika kuandaa Miongozo ya Kitaifa ya Shughuli za kushughulisha mwili, Miongozo ya Ulaji Unaotegemea Makundi ya Vyakula na Mwongozo wa Lishe Shuleni, pamoja na kuimarisha kanuni za kulinda unyonyeshaji.