WAZIRI MCHENGERWA AAGIZA UCHAMBUZI WA MAPITIO YA SHERIA YA FAMASI
Posted on: October 27th, 2026Na Clement Robert, WAF-Arusha
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, ameelekeza Baraza la Famasi kubainisha vifungu vya Sheria ya Famasi ya mwaka 2011 vinavyohitaji maboresho ili kuendana na maendeleo ya teknolojia, mahitaji ya viwanda vya dawa na mabadiliko ya taaluma.
Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 27, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 27 wa Mwaka na Kongamano la Kisayansi la TAPHATA jijini Arusha, akisisitiza umuhimu wa mifumo ya kisheria inayowezesha maendeleo ya sekta.
“Mapitio yazingatie teknolojia mpya, mahitaji ya viwanda na maslahi ya umma,” amesema Waziri Mchengerwa, akieleza vipaumbele vinavyopaswa kuongoza mchakato huo.
Ameitaka TAPHATA kuwasilisha mapendekezo yake kwa kubainisha vifungu vinavyohitaji marekebisho na sababu zinazounga mkono mapendekezo hayo ili kuwezesha uchambuzi wa kitaalamu.
Amesema mabadiliko ya teknolojia na upanuzi wa shughuli za uzalishaji wa dawa vinahitaji mifumo inayosimamia taaluma huku ikiwezesha ubunifu na maendeleo ya sekta.
Aidha, ameelekeza Wizara, Baraza la Famasi, TAPHATA na wadau husika kuchambua pendekezo la kuanzisha famasi jamii za Daraja la kwanza na pili kwa kuzingatia aina za huduma, sifa za watoa huduma na mahitaji ya usimamizi.
Amesisitiza kuwa mapitio ya sheria na uchambuzi wa mapendekezo hayo vinapaswa kulinda usalama wa wagonjwa na maslahi ya umma, huku vikiweka mazingira yanayowezesha uwekezaji na kujiajiri.