MHE. MCHENGERWA AAGIZA WIZARA YA AFYA KUPITIA MAAZIMIO YA TAPHATA NDANI YA SIKU 40
Posted on: October 27th, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Arusha
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, ameelekeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Mfamasia Mkuu wa Serikali kuratibu majadiliano na TAPHATA, Baraza la Famasi na Taasisi husika ili kufuatilia utekelezaji wa hoja zilizowasilishwa katika risala ya chama hicho.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 27 wa Mwaka na Kongamano la Kisayansi la TAPHATA jijini Arusha, leo Oktoba 27, 2026.
Amesema taarifa ya uchambuzi wa awali wa hoja hizo inapaswa kuwasilishwa Wizara ya Afya ndani ya siku 40 baada ya mkutano, huku kila hoja ikiainishiwa hatua za utekelezaji, muda na kipimo cha kupima maendeleo.
“Majibu haya yasiwe maneno ya siku moja,” amesema Waziri Mchengerwa, akihimiza umuhimu wa kufuatilia maelekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha yanazaa matokeo.
Amesema hoja zitakazofanyiwa uchambuzi ni pamoja na ajira za Wateknolojia Dawa, mapitio ya Sheria ya Famasi ya mwaka 2011, famasi jamii, maduka ya dawa muhimu na mazingira ya kazi ya wataalamu hao.
Hoja nyingine zinahusu uzalishaji wa dawa, kipaumbele kwa bidhaa za ndani, bima ya afya kwa Wateknolojia Dawa na uboreshaji wa mitaala ili kuendana na maendeleo ya teknolojia.
Ameelekeza kuwa masuala yanayohitaji mabadiliko ya sheria, bajeti au vibali yawasilishwe katika mamlaka zinazohusika, huku Wizara na wadau wakiendelea kushirikiana katika kutekeleza hatua zinazowezekana kwa mujibu wa taratibu zilizopo.