Ministry of Health

WATEKNOLOJIA DAWA WATAKIWA KUZINGATIA UBORA, MAADILI NA UBUNIFU

Posted on: October 27th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Arusha

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amewataka Wateknolojia Dawa nchini kuzingatia maadili ya taaluma, kuimarisha ubora wa huduma na kutumia ubunifu katika kutatua changamoto zinazohusu upatikanaji na matumizi sahihi ya dawa.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo Oktoba 27, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 27 wa Mwaka na Kongamano la Kisayansi la TAPHATA jijini Arusha, akisisitiza umuhimu wa wataalamu hao katika kulinda afya za wananchi.

Amesema Wateknolojia Dawa wana wajibu wa kuhakikisha dawa zinahifadhiwa katika mazingira yanayofaa, zinatolewa kwa usahihi na wagonjwa wanapata elimu kuhusu matumizi yake.

“Ilindeni taaluma kwa maadili, mafunzo endelevu na kuheshimu mipaka ya utendaji,” amesema Waziri Mchengerwa, akiwataka wataalamu hao kuzingatia misingi ya taaluma yao.

Aidha, amewataka kuimarisha kumbukumbu za ugavi wa dawa na kutoa taarifa za matatizo ya ubora kupitia mifumo inayotambuliwa na mamlaka husika ili kulinda usalama wa wagonjwa.

Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali, uchambuzi wa takwimu na akili unde yanaweza kusaidia kuboresha huduma, akisisitiza kuwa teknolojia hizo zitumike kwa kuzingatia usahihi wa taarifa, faragha na usalama wa wagonjwa.

Amekihimiza TAPHATA kushirikiana na vyuo na wataalamu wa kada nyingine katika tafiti na miradi ya ubunifu inayoweza kupunguza upotevu wa dawa, huku akisisitiza kuwa uadilifu, ubora na ubunifu ni nguzo za maendeleo ya taaluma.