Ministry of Health

SERIKALI KUWEKA MSUKUMO KATIKA UZALISHAJI WA DAWA NCHINI

Posted on: October 27th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Arusha

Serikali imesisitiza dhamira ya kukuza uzalishaji wa dawa nchini kwa kuweka mazingira yatakayowezesha viwanda vya ndani kukua, kuongeza ajira na kuboresha upatikanaji wa dawa bora kwa wananchi.

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema uzalishaji wa ndani wa dawa na bidhaa za afya ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 27 wa Mwaka na Kongamano la Kisayansi la TAPHATA jijini Arusha Oktoba 27, 2026, amesema Serikali imechukua hatua za kuharakisha uwekezaji katika viwanda vya dawa, ikiwamo kuanzishwa kwa Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Viwanda vya Dawa (PIAT).

“Usimamizi wa viwango si kikwazo cha ukuaji; ndiyo ulioifanya nchi ya China iaminiwe,” amesema Waziri Mchengerwa, akisisitiza umuhimu wa mifumo imara ya udhibiti wa ubora na usalama wa dawa.

Ameeleza kuwa mafanikio ya sekta hiyo yanahitaji ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za elimu, wadhibiti, wawekezaji na wataalamu ili kuhakikisha dawa zinazozalishwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Aidha, ameelekeza Wizara ya Afya, MSD na wadau wa uzalishaji kuchambua fursa na changamoto za masoko kwa dawa za ndani, huku utaratibu wa kutoa kipaumbele ukizingatia sheria za ununuzi, ubora, bei na uhakika wa upatikanaji.

Amesisitiza kuwa kuimarisha uzalishaji wa ndani ni muhimu katika kujenga uwezo wa Tanzania katika sekta ya dawa, kupanua ajira na kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.