Ministry of Health

KUPUNGUZA MATUMIZI YA CHUMVI, SUKARI NA MAFUTA, KUFANYA MAZOEZI NI MSINGI WA AFYA BORA

Posted on: October 29th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amewataka wananchi kupunguza matumizi ya sukari, chumvi na mafuta katika vyakula pamoja na kuepuka tabia bwete ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha afya zao.

Dkt. Magembe amesema hayo leo Oktoba 29, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa 2026 yanayofanyika mkoani Dodoma, yenye kaulimbiu isemayo, “Imarisha Afya, Kula Kiasili, Punguza Sukari, Punguza Mafuta na Chumvi.”

"Nitoe rai kwa wananchi kuzingatia ulaji wa mlo kamili wenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya vyakula, Tanzania ina utajiri wa vyakula vya asili ikiwemo nafaka, mizizi, mboga za majani, matunda na vyakula vingine vyenye virutubisho muhimu kwa afya ya binadamu," amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema changamoto kubwa si ukosefu wa vyakula nchini, bali ni maamuzi yanayofanywa na wananchi katika kuchagua vyakula wanavyotumia kila siku, hivyo amewahimiza kupendelea vyakula vya asili na vyenye virutubisho, kupunguza matumizi yaliyokithuri ya sukari, chumvi na mafuta.

Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amewahimiza wananchi kushuhulisha miili na kuepuka tabia bwete kwa kukaa bila kufanya mazoezi ambapo kunachangia ongezeko la uzito na hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.

Vilevile, Dkt. Magembe amewataka wazazi na walezi kuwa mfano bora kwa watoto katika uchaguzi wa vyakula na mtindo bora wa maisha, akibainisha kuwa watoto hujifunza tabia za ulaji kutoka kwa watu wazima.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kupunguza matumizi ya mara kwa mara ya pipi, soda, aiskrimu juisi zisizo halisi, vinjwaji vya kuongeza nguvu (energy drinks), chipsi na vyakula vingine vyenye sukari na mafuta mengi ili kulinda afya za watoto tangu wakiwa wadogo.

Akihitimisha hutuba yake, Dkt. Magembe amesema juhudi za kuboresha lishe zinapaswa kuambatana na mabadiliko ya tabia na ushirikiano wa familia, wataalamu wa afya na wadau mbalimbali ili kujenga jamii yenye afya bora na kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini.