Ministry of Health

LISHE BORA MSINGI WA AFYA NA MAENDELEO YA TAIFA

Posted on: October 29th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma

Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa Dkt. Vida Mmbaga amesisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya lishe bora na kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha wananchi kupata na kuchagua vyakula bora na salama ili kukabiliana na changamoto za lishe nchini.

Dkt. Mmbaga amesema hayo leo Oktoba 29, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa 2026 yanayofanyika mkoani Dodoma, ambapo mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe.

"Tanzania bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali za lishe, zikiwemo udumavu kwa watoto, upungufu wa damu pamoja na ongezeko la uzito uliozidi na unene uliokithiri miongoni mwa wanawake na watoto," amesema Dkt. Mmbaga

Aidha, Dkt. Mmbaga amesema kuwa takribani asilimia 30 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wana udumavu, huku upungufu wa damu ukiwaathiri asilimia 59 ya watoto wa umri huo na asilimia 42 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa, kati ya miaka 15 na 49.

"Uzito uliozidi na unene uliokithiri huongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kiharusi, magonjwa ya figo na baadhi ya saratani, hivyo kuhitaji juhudi za pamoja katika kuzuia na kukabiliana na hali hiyo," amesema Dkt. Mbaga

Pia, Dkt. Mmbaga ameeleza kuwa lishe bora ni muhimu kwa ukuaji wa watoto, maendeleo ya ubongo, uwezo wa kufikiri na mahudhurio mazuri shuleni, huku kwa vijana balehe ikiweka msingi wa afya njema wanapokuwa watu wazima.

Hata hivyo, amesema ni asilimia 18 pekee ya watoto wenye umri wa miezi sita hadi 23 wanaopata mlo wenye mchanganyiko wa kutosha wa makundi mbalimbali ya vyakula, huku asilimia 97 ya Watanzania hawatumii kiwango kinachopendekezwa cha matunda na mboga kwa siku.

Dkt. Mbaga amehitimisha kwa kusisitiza kuwa elimu ya lishe inapaswa kuambatana na uwepo wa mazingira wezeshi yanayorahisisha upatikanaji wa vyakula bora na salama, akitoa wito kwa sekta mbalimbali kushirikiana katika kuboresha hali ya lishe nchini.