WIZARA YA AFYA YAENDELEA KUIMARISHA UTAYARI WATAALAM WA MAABARA NCHINI
Posted on: September 16th, 2026Na Zakayo Mosha-WAF MWANZA
Wizara ya Afya kupitia Idara ya huduma za Uchunguzi wa Magonjwa, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO),inaendesha mafunzo kwa Wataalam wa Maabara kwa lengo la kuimarisha utayari, usimamizi sampuli pamoja na utoaji wa taarifa sahihi za magonjwa ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko nchini.
Akifungua mafunzo hayo leo Septemba 16, 2026, Mkoani Mwanza, Dkt.Kheri Kagya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ametoa pongezi na shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kufanikisha utoaji wa mafunzo hayo muhimu ya Wataalam wa Maabara kufanyika Mkoani Mwanza.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi hapa nchini katika utoaji wa huduma bora za afya,amesisitiza Serikali haishindani na Sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya ,badala yake pande zote mbili zinashirikiana kikamilifu ili kutoa huduma bora za afya kwa mwananchi.
"Napenda kutoa rai kwa Wataalam wa Maabara mnaoendelea kushiriki mafunzo haya ya siku tano yaliyoanza septemba 14 hadi 18, 2026 kutumia vema ujuzi na maarifa mapya mtakayopata hapa, kwenda kushirikiana na Wataalam wengine waliobaki vituo vya kazi ili kwa pamoja muimarishe utoaji wa huduma za afya kwa Wananchi" amesema Dkt.Kheri
Ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imeendelea kuboresha ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa hususani vifaa vya Maabara, amefafanua kuwa vifaa hivyo vimesambazwa na vinatumika katika Hospitali za Rufaa za Mikoa,Hospitali za Wilaya na katika vituo vya Afya hapa nchini.
Awali akizungumza Bw. Salum Nyanga mtaalam kutoka Maabara ya Taifa ambaye pia ni Meneja msaidizi Maabara ya Taifa afya ya jamii, amesema Serikali ya awamu ya Sita imejiimarisha zaidi kwa vifaa vya kisasa vya Maabara, ambapo vipimo vya Sampuli zote za Magonjwa vinafanyika hapa nchini na kuwezesha Serikali kuokoa fedha za kupata huduma hizo nje ya nchi.