Ministry of Health

WASHAWISHI WA MITANDAO YA KIJAMII KUUNGANA KUCHOCHEA UELEWA WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: November 12th, 2026

Na WAF-Dar es Salaam

Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha matumizi ya majukwaa ya kidijitali katika kuelimisha wananchi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kupitia mkutano wa uelekezaji kwa washawishi wa mitandao ya kijamii uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umewakutanisha washawishi mbalimbali wa mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu kampeni ya Bima ya Afya kwa Wote na kuwapa mwongozo wa namna bora ya kutumia ushawishi na majukwaa yao kufikisha elimu kwa wananchi, hususan kuhusu kifurushi cha Fahari Afya.

Akizungumza katika mkutano huo leo Novemba 11, 2026, Mratibu wa Elimu ya Afya wa Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, Said Makora, amesema washawishi wa mitandao ya kijamii wana nafasi muhimu katika kuhamasisha wananchi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kwa kutumia lugha rahisi na njia zinazoweza kueleweka na makundi mbalimbali ya jamii.

Amesisitiza umuhimu wa washawishi kuwa na uelewa sahihi kuhusu kampeni hiyo ili waweze kutoa taarifa sahihi, kujibu maswali ya wananchi na kuondoa dhana potofu zinazoweza kujitokeza kuhusu bima ya afya.

Kwa upande wake, Afisa Programu wa Mawasiliano ya Afya na Mabadiliko ya Tabia kutoka Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Simwanza Mrisho, amesema matumizi ya mawasiliano yenye ushawishi ni muhimu katika kuhamasisha mabadiliko chanya ya tabia na kuongeza mwitikio wa wananchi katika masuala ya afya.

Ameeleza kuwa washawishi wa mitandao ya kijamii wana nafasi muhimu katika kufikisha ujumbe wa afya kwa jamii kutokana na ushawishi wao kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.

Kupitia ushiriki wa washawishi hao, kampeni inalenga kutumia nguvu ya mawasiliano ya kidijitali kufikisha elimu kwa wananchi wengi zaidi, kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya na kujenga mtazamo chanya kuhusu maandalizi ya kifedha kwa ajili ya huduma za afya.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza ufahamu wa wananchi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote na umuhimu wa kila mmoja kuchukua hatua za mapema katika kulinda afya yake na ustawi wa familia.