VIFAA TIBA VYA TSH.BILIONI 1.2 KUIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA YA UZAZI NA WATOTO WACHANGA
Posted on: November 12th, 2026Na Mvuda Jaffer, WAF – Arusha
Serikali imekabidhi vifaa tiba 396 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa vituo 140 vya kutolea huduma za afya katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Lindi, kwa lengo la kuimarisha huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga (CEmONC).
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo leo Novemba 12, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba A. Nguvila, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, amesema vifaa hivyo vimenunuliwa kupitia Mradi wa ACHIEVE unaotekelezwa na Taasisi ya Pact Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani.
"Mradi huu pia umechangia kuimarisha uwezo wa watumishi wa Afya 407 kupitia mafunzo ya vitendo, ushauri elekezi na ufuatiliaji wa utoaji wa huduma," amesema Dkt. Nguvila
Ameeleza kuwa vifaa hivyo vinajumuisha mashine za kuongeza joto kwa watoto wachanga (Infant Radiant Warmers), kudhibiti utoaji wa dawa na vimiminika mwilini (Infusion Pumps) na kusaidia upumuaji wa watoto wachanga (CPAP Machines).
Pia, Dkt. Nguvila amesisitiza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua, ili kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma bora na salama.
Aidha, Dkt. Nguvila amesema afya ya mama na mtoto ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuwekeza katika huduma za uzazi, miundombinu na vifaa tiba.
Vilevile, amewataka watumishi wa afya kutumia na kutunza vifaa hivyo kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa ili viweze kutoa huduma iliyokusudiwa na kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Katika hatua nyingine, ametoa shukrani kwa Serikali ya Marekani kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Misaada ya Nje kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, TAMISEMI na mamlaka za afya katika kufanikisha mradi huo, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini.