SERIKALI KUTOA HUDUMA ZA UPASUAJI WA MABUSHA KWA WAGONJWA 2,000 BURE
Posted on: November 14th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Mlandizi, Pwani.
Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence George Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutoa huduma za upasuaji wa mabusha (Ngirimaji) kwa wagonjwa 2,000 bila malipo katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini.
Dkt. Samizi ameyasema hayo Novemba 14, 2026, wakati akitembelea kambi ya upasuaji wa mabusha katika eneo la Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, ambapo ametoa wito kwa wananchi wenye tatizo hilo kujitokeza kupata uchunguzi na matibabu yanayotolewa bure na Serikali.
Amesema huduma hizo zitatolewa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ya Novemba hadi Desemba 2026 inalenga kuwahudumia wagonjwa 1,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga na Mbeya.
Ameeleza kuwa hadi Novemba 14, 2026, katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Mbeya, jumla ya wananchi 533 wamefanyiwa uchunguzi, ambapo wagonjwa 315 wamebainika kuwa na tatizo la mabusha na kati yao 182 tayari wamefanyiwa upasuaji na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Aidha, amesema kambi ya upasuaji katika Mkoa wa Tanga inatarajiwa kuanza Novemba 16, 2026, katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, ili kuwawezesha wananchi wenye tatizo hilo kupata huduma karibu na maeneo yao.
Dkt. Samizi amesema matende na mabusha ni magonjwa yanayoenezwa na mbu na yanaweza kusababisha ulemavu pamoja na changamoto za kiafya na kijamii endapo hatua za matibabu hazitachukuliwa kwa wakati.
Amesema kwa wanaume wenye tatizo la mabusha, upasuaji ndiyo tiba inayoweza kurekebisha hali hiyo, kuwawezesha kurejea katika shughuli zao za kila siku na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya familia.
Dkt. Samizi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kinga na tiba, ikiwemo huduma za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.