Ministry of Health

TANZANIA YAIMARISHA RASILIMALI ZA NDANI KUGHARAMIA HUDUMA ZA AFYA NA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

Posted on: November 12th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Durban, Afrika Kusini.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Tanzania yaimarisha rasilimali za ndani kwa ajili ya kugharamia huduma za afya na afua za mapambano dhidi ya UKIMWI, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya ufadhili wa afya kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Dkt. Samizi amebainisha hayo leo Novemba 12, 2026, jijini Durban nchini Afrika Kusini, katika kikao cha Mawaziri wa Afya na wenye dhamana ya masuala ya UKIMWI wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa majadiliano kuhusu tathmini ya hali ya magonjwa katika ukanda huo (Epidemiological Outlook of the SADC Region).

Dkt. Samizi amesema Tanzania inatambua hali ya magonjwa katika ukanda wa SADC pamoja na juhudi zinazofanywa na baadhi ya nchi wanachama katika kufikia malengo yaliyowekwa ya kuboresha afya za wananchi.

Amesema kufuatia changamoto ya ufadhili wa sekta ya afya iliyojitokeza mwaka 2024 baada ya kusitishwa kwa ufadhili kupitia Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR), Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuimarisha uwezo wa ndani wa kugharamia huduma za afya.

Ameeleza kuwa miongoni mwa mikakati hiyo ni kuwa na mfuko Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote, huku Serikali ikiweka Mfuko Maalumu wa Usawa (Equity Fund) kwa ajili ya kusaidia kaya maskini na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi kupata huduma za afya.

Aidha, amesema wananchi wenye uwezo wa kuchangia wanapata fursa ya kujiunga na mfuko huo kwa kujilipia wenyewe, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika kugharamia huduma za afya.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema Serikali imeweka utaratibu wa kutumia mapato yanayokusanywa kupitia kodi za ndani kugharamia huduma za afya, ambapo asilimia 30 ya fedha hizo zinaelekezwa katika Bima ya Afya kwa Wote, huku asilimia 70 zikitumika kugharamia afua za mapambano dhidi ya UKIMWI.