MWANZA YAZINDUA MRADI WA MSINDIKIZI WA MAMA MJAMZITO KUBORESHA HUDUMA ZA UZAZI
Posted on: November 13th, 2026Na Zakayo Mosha, WAF – Mwanza
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na Shirika la Thamini Uhai Tanzania, imezindua mradi wa msindikizaji wa mama mjamzito (Birth Companionship) katika vituo 12 vya kutolea huduma za afya mkoani Mwanza. Mradi huo unalenga kuimarisha huduma za uzazi zinazozingatia utu, heshima, faragha na usalama wa mama na mtoto.
Akiongea katika uzinduzi huo uliofanyika leo Novemba 13, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Fatuma Mganga, amesema msindikizaji wa mama mjamzito hapaswi kuwa muhimu wakati wa kujifungua pekee, bali katika kipindi chote cha ujauzito ili kumsaidia mama kukabiliana na changamoto na dharura zinazoweza kujitokeza.
"Baadhi ya wajawazito hukabiliwa na changamoto za kiafya, kijamii na kisaikolojia, ikiwemo kukosa msaada wa karibu kutoka kwa familia. Amewataka viongozi wa halmashauri na watendaji wa afya kuhakikisha huduma hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia heshima na faragha, sambamba na kuboresha vyumba vya kujifungulia", amesema Dkt.Mganga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Thamini Uhai Tanzania, Bw. Banzi Msumi, amesema mradi huo ulianza kwa majaribio mwaka 2017 kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Geita, kabla ya kuanza kutekelezwa mkoani Mwanza mwaka 2023. ameeleza kuwa mradi huo pia umewasilishwa katika Kamati ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI kwa ajili ya kuwajengea wajumbe uwezo wa kusimamia utekelezaji na uendelevu wake.
Aidha, Bw. Msumi amesema Mkoa wa Mwanza bado unakabiliwa na changamoto ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga, hivyo amewaomba wadau wengine wa afya kuongeza kushirikiana na Serikali, kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na dharura za uzazi na kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa Wananchi.
Naye msimamizi wa huduma za afya zinazozingatia utu, heshima na staha kutoka Wizara ya Afya, Bi. Fidea Obimbo, ameipongeza Thamini Uhai Tanzania kwa kushirikiana na Serikali katika kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto nchini.