Ministry of Health

TANZANIA YASAINI HATI YA MAKUBALIANO YA UNUNUZI WA PAMOJA WA DAWA NA VIFAA TIBA

Posted on: November 12th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Durban, Afrika Kusini.

Tanzania imesaini Hati ya Makubaliano ya kuanzisha Mpango wa Ununuzi wa Pamoja wa Dawa na Vifaa Tiba wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), huku ikikubali kuwa mwenyeji wa mpango huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba bora, salama na kwa gharama nafuu katika ukanda huo.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania inaunga mkono kikamilifu uanzishwaji na utekelezaji wa mpango huo na ipo tayari kutekeleza wajibu wake kama mwenyeji kwa kushirikiana na nchi wanachama.

Amesema kuunganisha mahitaji ya nchi wanachama kutatoa soko la uhakika kwa wazalishaji wa dawa na vifaa tiba, kuongeza uwezo wa kupata bidhaa kwa gharama nafuu na kuchochea uwekezaji katika viwanda vya dawa barani Afrika.

Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizokubali kushiriki katika mpango huo ni Afrika Kusini, Lesotho na Msumbiji, hatua inayodhihirisha dhamira ya nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Aidha, Dkt. Samizi ameeleza kuwa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wa kisiasa, kitaasisi na rasilimali zinazohitajika ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa nchi za SADC.

Mpango huo wa SADC Pooled Procurement Services (SPPS) unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za afya na kuboresha mifumo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika nchi wanachama.