Ministry of Health

KAMBI YA UPASUAJI WA MABUSHA/NGIRIMAJI KUTOA HUDUMA BURE TANGA

Posted on: November 12th, 2026

Na Alex Nkondo, WAF – Tanga

Wananchi wa Mkoa wa Tanga wanatarajiwa kunufaika na huduma za upasuaji bila malipo kupitia Kambi Maalumu ya Upasuaji wa Mabusha na Ngirimaji itakayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 30 Novemba 2026, katika Wilaya za Handeni, Muheza na Korogwe.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema Serikali itagharamia huduma hizo ili kuwawezesha wananchi wenye matatizo ya mabusha na ngirimaji kupata uchunguzi na matibabu stahiki bila malipo.

Amesema kambi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa na upasuaji karibu na wananchi, hususan wale wanaokabiliwa na changamoto za kupata huduma hizo kutokana na gharama na umbali wa vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, ameeleza kuwa upatikanaji wa huduma hizo utasaidia kupunguza madhara yanayotokana na matatizo ya mabusha na ngirimaji, ambayo yanaweza kuathiri afya, uwezo wa kufanya shughuli za kiuchumi na ustawi wa wananchi.

Dkt. Burian amewahimiza wananchi wenye matatizo hayo kujitokeza kwa wingi katika vituo vitakavyotengwa kwenye wilaya husika ili kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu kulingana na ushauri wa wataalamu wa afya.

Kambi hiyo inatarajiwa kuongeza fursa kwa wananchi wa Wilaya za Handeni, Muheza na Korogwe kupata huduma za upasuaji kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.