Ministry of Health

WANANCHI TANGA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUPATA MATIBABU YA MABUSHA NA NGIRIMAJI BILA MALIPO

Posted on: November 16th, 2026

Na Alex Nkondo, WAF – Handeni, Tanga.

Wananchi wenye changamoto za mabusha na ngirimaji mkoani Tanga wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika kambi maalumu iliyoanza rasmi mkoani humo.

Wito huo umetolewa leo tarehe 16 Novemba, 2026 na Mganga mkuu wa wilaya, Dkt. Kisaka kachua, alipokutana na timu ya wataalamu wa Afya wanaohudumu katika kambi ya Mabusha/Ngirimaji Mkoani Tanga.

Dkt. kachua amesema wananchi hawapaswi kuwa na hofu ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu, kwani timu ya wataalamu wa afya imejipanga kuhakikisha huduma zinatolewa kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia taratibu za kitaalamu.

"Utekelezaji wa kambi hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kupunguza madhara yatokanayo na Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu na kuimarisha afya na ustawi wa wananchi'," Ameongeza

Kwa upande wake, Afisa Afya na Mratibu wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Bw. Godfrey Ngariba, amewataka wananchi wenye dalili au changamoto za mabusha na ngirimaji kutumia fursa hiyo kupata uchunguzi na matibabu stahiki badala ya kuendelea kuishi na matatizo hayo bila kutafuta msaada wa kitaalamu.

Aidha, amewahimiza wananchi kushirikiana katika kusambaza taarifa kuhusu uwepo wa kambi hiyo ili kuwafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji wa huduma, hususan wale ambao wamekuwa wakishindwa kupata matibabu kwa wakati.

Kambi hiyo inalenga kuwahudumia wagonjwa zaidi ya 1,000, huku timu ya wataalamu wa afya ikiwa imefanya maandalizi ya kuhakikisha wananchi wanaojitokeza wanapata huduma kulingana na mahitaji yao.