Customer Feedback Centre

Ministry of Health

NEC WAPITISHA MAPENDEKEZO YA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: June 23rd, 2022

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM (NEC) leo Juni 23 2022 wamepitisha kwa kishindo mapendekezo ya Bima ya Afya kwa wote nchini.
Wajumbe hao wamepitisha mapendekezo hayo kwenye semina iliyoandaliwa na Wizara ya Afya ya kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini iliyofanyika kwenye ukumbi wa White house jijini Dodoma.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hatua hiyo inapelekea Wizara ya Afya kwenda kutunga sheria ya Bima ya Afya kwa wote na kuongeza kuwa kiasi kitakacholipwa na mwananchi kwa mwaka atapata huduma za matibabu kama mtumishi wa Serikali, kuanzia ngazi ya Zahanati, Kituo cha Afya, hospitali ya Wilaya, Rufaa za Mkoa, Kanda, Maalumu na hata Taifa ya Muhimbili.

“Hii itasaidia kwa Watanzania wote kupata huduma bora za Afya bila kikwazo cha fedha pia Serikali itahakikisha Dawa zinapatikana kwa wakati na zinazokidhi mahitaji ya wagonjwa”. Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema kuwa na bima ya afya kwa wote ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, Ibara ya 83(e) cha kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwemo mifuko ya bima za afya (NHIF na CHF) ili kufikia lenho la Serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote