Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ZAIDI YA FAMILIA 760 HANANG ZAPATIWA ELIMU YA KUJIKINGA NA MAGONJWA YA MLIPUKO.

Posted on: December 8th, 2023


Na. WAF,  Hanang 

Serikali imesema Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wametoa elimu kwa Familia zaidi ya 760 juu ya kutumia dawa ya kutibu maji ili  kuzuia Magonjwa ya mlipuko kipindi  hiki  cha maafa katika mji mdogo wa Katesh Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara.

Hayo yamesemwa Leo Disemba 8, 2023 Wilayani Hanang na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akizungumza  na Waandishi wa habari baada ya  kufanya kikao cha kuwashukuru Wadau pamoja na watu wengine ambao wamekuwa bega Kwa bega na Serikali katika utoaji wa huduma na misaada kwa Waathirika wa Mvua ya Mafuriko.

"Tumeleta dawa za kutibu maji, katika kuhakikisha tunaimarisha suala la Kinga dhidi ya Magonjwa ya mlipuko tayari Wahudumu wa Afya wamefikia familia  760 kutoa elimu  namna ya  Matumizi ya dawa ya kutibu maji na hii itasaidia kwenye suala la kuzuia Magonjwa yatokanayo na maji ikiwemo kuhara hivyo tumejipanga Ili suala hili la Mafuriko lisilete balaa jingine". Amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel amesema asilimia 98% ya Majeruhi ambao ilitakiwa wakatiwe rufaa wametibiwa ndani ya Mkoa wa Manyara hii ni kutokana na Serikali kujipanga vyema kuhakikisha kuwa huduma za kibingwa  zimeimarishwa ili kuokoa uhai.

"Huduma za kibingwa zimesogezwa hapa, timu ya Madaktari bingwa wameweka Kambi mkoa wa Manyara ambapo asilimia 98 ya Wagonjwa waliotakiwa wakati Rufaa wanatibiwa hapa Manyara". Amesema.

Halikadhalika, Dkt. Mollel amewashukuru Wadau kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kukabiliana na maafa yaliyotikea Katesh.

"Tunashukuru sana wadau na watu wengine kwa kuendelea kutoa ushirikiano yaani mmefanya kazi nzuri sana". Amesema.