Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAONGEZA KASI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA MAGONJWA YASIYOPEWA KIPAUMBELE

Posted on: January 25th, 2024


NA: WAF, Dar Es Salaam

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeongeza kasi ya kutoa elimu na dawakinga kwa jamii ili kuyatokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele ifikapo 2030.

Yameelezwa hayo na Afisa Programu kutoka Mpango wa Taifa wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele Wizara ya Afya Dkt. Isaac Njau katika semina ya waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele Duniani (matende na mabusha, Usubi, Trakoma, Kichocho na Minyoo ya tumbo) inayotarajiwa kufanyika Januari 30, mwaka huu.

“Mwaka huu tumejipanga kuadhimisha Siku ya Magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, maadhimisho yatafanyika ngazi za mikoa na halmashauri kwa kutoa elimu na hamasa juu ya magonjwa haya katika jamii." Amesema.

Dkt. Clara Mwansasu ni Afisa kutoka Mpango huo wa kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele ameeleza kuwa, Tanzania imekuwa ikitekeleza afua za kutokomeza magonjwa hayo ikiwemo kutoa elimu na kumezesha dawa (NTD’s) baada ya kuwa imefanya tathmini ya kina.

Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushiriki katika utekelezaji wa afua nyinginezo ikiwemo usafi wa mazingira na mwili kwani ni moja ya visababishi vikubwa vya magonjwa yasiyopewa kipaumbele.