Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAFANYA MABADILIKO YA UONGOZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA TANGA-BOMBO.

Posted on: January 23rd, 2024



Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya mabadiliko ya kiuongozi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo ikiwa na lengo la kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma bora za Afya kwa Watanzania.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali Watu Wizara ya Afya Bw. Danny Temba wakati wa halfa ya makabidhiano ya ofisi kwa Mganga Mfawidhi Mpya Dkt. Frank Shega kutoka kwa aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt. Naima Yusuf katika Hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeo.

Alisema Serikali inayoongozwa na Rais. Dkt. Samia Suluhu kwa kipindi cha muda mfupi imefanya maboresho makubwa sana kwenye sekta ya Afya katika maeneo ya miundombinu,vifaa tiba na watumishi, Hivyo mabadiliko ya Uongozi huo unalenga kuzidi kuleta mapinduzi kwenye utoaji wa huduma bora kwa wananchi .

“Kutokana na maboresho yaliyofanywa na Mhe. Rais. Dkt. Samia katika sekta ya Afya, Watumishi wote tunadeni la kutimiza wajibu wetu wa kuhakikisha tunawapatia wananchi huduma bora za Afya pia kupitia mabadiliko haya ya uongozi tunategemea kila mmoja wetu ashirikiane na uongozi wa ndani na nje ya Wizara kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na bora kwa watanzania kwa kuwa utaalamu wetu unategemewa sana na wananchi. ” Alisema Bw. Temba.

Awali akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo Mganga Mfawidhi mpya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Dkt. Frank Shega aliomba ushirikiano kwa sababu wanakwenda kufungua ukurasa mwingine wa kiutendaji wenye lengo la kuboresha huduma na kuzitaka Timu ya Viongozi wa Hospitali (RRHMT) na Timu ya Uongozi wa Afya Mkoa (RHMT) kushirikiana ili kwa pamoja kuweza kufikia malengo yaliyowekwa kwa wakati.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeo alisema Dkt. Naima anayemaliza muda wake amefanya kazi kubwa sana kwa kujitahidi kubuni vitu mbalimbali ili kuhakikisha wanaongeza mapato kwenye Hospitali hiyo.