WIZARA YA AFYA NA TAMISEMI ZABAINISHA MIKAKATI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI
Posted on: February 13th, 2026Na WAF-DODOMA,
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI zimekutana na Kamati za Kudumu za Bunge za Afya na Masuala ya UKIMWI pamoja na TAMISEMI na kubainisha mikakati ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya hadi ngazi ya msingi, ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha sekta hiyo nchini.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Februari 13, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza vya kutosha katika kuboresha huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora na kwa wakati.
Dkt. Samizi amesema maboresho hayo yanahusisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba vya kisasa pamoja na upatikanaji wa dawa katika ngazi zote kuanzia zahanati, vituo vya afya hadi hospitali za rufaa, kanda hadi kitaifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Rajab Seif, amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha huduma za afya zinawafikia walengwa kwa ubora unaokusudiwa, sambamba na kuimarisha usimamizi na uratibu katika mamlaka za serikali za mitaa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, ameipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua zilizofikiwa katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, akieleza kuwa ameridhishwa na uwepo wa vifaa, dawa na miundombinu inayokidhi mahitaji katika maeneo ya msingi.
Ameitaka Wizara ya Afya na TAMISEMI kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha huduma bora zinaimarika zaidi, hatua itakayosaidia kufikia malengo ya muda mrefu ya taifa ya kuhakikisha afya za Watanzania zinaendelea kuimarika kuelekea mwaka 2050.