Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAELEKEZA MIKAKATI MIPYA KUWAFIKIA WATOTO WANAOKOSA CHANJO

Posted on: June 4th, 2026

Na Mvuda Jaffer,WAF-Dar es Salaam

Wizara ya Afya imezitaka Mikoa na Halmashauri nchini kuimarisha huduma za chanjo kwa kubuni mbinu mpya za kuwafikia watoto ambao hawajapata chanjo kabisa (zero-dose) au ambao hawajakamilisha ratiba za chanjo, ili kuongeza kinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Maelekezo hayo yametolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dkt. Hamad Nyembea, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Huduma za Chanjo nchini unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt.Nyembea amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa huduma za chanjo kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo ambapo walengwa zaidi ya asilimia 80 wameendelea kufikiwa, bado kuna makundi ya watoto katika jamii za wafugaji, wavuvi, maeneo ya migodini pamoja na baadhi ya maeneo ya mijini ambayo hayajafikiwi kikamilifu na huduma hizo.

“Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa Chanjo wa mwaka 2026–2030 unaolenga kuhakikisha huduma za chanjo zinawafikia walengwa wote na kujenga jamii yenye kinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.”amesema Dkt.Nyembea

Aidha, Dkt.Nyembea ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwemo Surua na Polio, hali inayosababisha kushindwa kuwabaini mapema wahisiwa wa magonjwa hayo na kuchukua hatua stahiki za kinga na udhibiti.

“Wizara ya Afya imezitaka Halmashauri na vituo vya kutolea huduma za afya kutumia kikamilifu fursa ya usafirishaji wa sampuli kupitia Shirika la Posta pamoja na kutenga rasilimali kwa ajili ya uibuaji wa wahisiwa, uchukuaji wa sampuli na usafirishaji wake ili kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa hayo.”amesema Dkt. Nyembea

Pia Dkt.Nyembea amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za mkoba na huduma tembezi katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya, akieleza kuwa huduma hizo ni nyenzo muhimu ya kuwafikia walengwa ambao hawawezi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.