Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA WADAU KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: November 5th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zinazokidhi mahitaji yao.

Hayo yamesemwa leo tarehe 04 Novemba, 2026, Mkoani Dar es salaam, na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti, Bw. Mintanga Milulu, wakati wa Kikao cha Ushauri wa Wadau kuhusu Rasimu ya “National Health Compact” yaani Makubaliano ya Kitaifa ya Afya wa Mwaka 2026/27–2030/31, kilicholenga kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau kwa ajili ya kuboresha rasimu hiyo.

Bw. Milulu ameeleza umuhimu wa Makubaliano hayo katika kuweka mfumo madhubuti ya uratibu wa rasilimali za sekta ya afya, ikiwemo kuoanisha mipango na bajeti za Serikali na wadau wa maendeleo ili kupunguza mwingiliano wa afua, kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha na kuhakikisha rasilimali zinaelekezwa katika maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathmini na uwajibikaji kupitia viashiria vinavyopimika, ukusanyaji wa takwimu sahihi na tathmini za mara kwa mara ili kufuatilia utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya afya na kupima matokeo ya uwekezaji katika huduma za afya.

Amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi za kidini, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji wa huduma za afya, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wenye malengo ya pamoja na mgawanyo wa majukumu unaoeleweka.