Wizara Ya Afya

WATAALAMU WA LISHE WATAKIWA KUONGEZA JUHUDI ZA KUTOA ELIMU YA LISHE BORA KWA JAMII Na

Posted on: November 5th, 2026

 Mvuda Jaffer, WAF-Morogoro


Wataalamu wa lishe nchini wametakiwa kuongeza juhudi katika kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa watoto wenye umri wa miezi sita na kuendelea, ili kuboresha afya na ukuaji wa watoto na kujenga jamii yenye afya bora.


Wito huo umetolewa leo Novemba 5, 2026 mkoani Morogoro na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kinga, Dkt. Vida Mmbaga wakati akizungumza katika kikao kazi cha pamoja cha wadau wa lishe kinachofanyika kupitia Programu ya First Food Tanzania, kinacholenga kujadili na kubuni mikakati ya elimu na uhamasishaji kuhusu ulishaji bora wa watoto.


Dkt. Mmbaga amewataka Maafisa Lishe kutumia nafasi zao kuelimisha jamii kuhusu namna bora ya kuandaa na kuwapatia watoto vyakula vyenye virutubishi vinavyohitajika kwa ukuaji na maendeleo yao akisisitiza kuwa elimu sahihi ya lishe ni msingi muhimu katika kukabiliana na changamoto za utapiamlo kwa watoto.


Aidha, amebainisha baadhi ya changamoto zinazoathiri upatikanaji wa lishe bora kwa watoto kuwa ni pamoja na upatikanaji wa elimu sahihi kutokana na kuwepo kwa watu wanaotoa elimu ya lishe bila kuwa na uelewa au utaalamu stahiki, changamoto ya muda unaohitajika kuandaa milo yenye mchanganyiko sahihi wa virutubishi pamoja na hali ya kiuchumi ya kaya.