RAI YATOLEWA KWA WANANCHI KUZINGATIA MITINDO BORA YA MAISHA
Posted on: November 9th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amewahimiza wananchi kuendelea kuzingatia mitindo bora ya maisha kwa kufuata kanuni za ulaji unaofaa, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara na kuepuka matumizi ya bidhaa zenye sukari nyingi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Prof. Sunguya ametoa rai hiyo wakati akitoa tamko kwa umma kuhusu wiki ya magonjwa yasiyoambukiza nchini mbele ya waandishi wa habari leo Novemba 09, 2026, jijini Dar es salaam, amesisitiza umuhimu wa wananchi kula mlo kamili wenye makundi yote sita ya vyakula, kuongeza ulaji wa mboga za majani na matunda, kupunguza matumizi ya chumvi na sukari, pamoja na kufanya mazoezi ya mwili kwa angalau dakika 30 kwa siku, siku tano kwa wiki.
Aidha, Prof. Sunguya amewataka wananchi kupata usingizi wa kutosha wa angalau saa nane kwa siku, kuepuka matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe kupita kiasi, pamoja na kujenga utamaduni wa kupima afya angalau mara moja kwa mwaka hata kama hawana dalili za ugonjwa.
Katika hatua nyingine, Prof. Sunguya amewataka wananchi kuepuka matumizi yaliyokithiri ya viburudisho vyenye sukari nyingi vinavyotolewa katika matamasha, mikutano, semina na warsha, ikiwemo pipi, biskuti, vinywaji baridi na sharubati zilizoongezewa sukari.
Badala yake, amehimiza matumizi ya viburudisho vyenye afya zaidi kama matunda, maji safi ya kunywa, karanga na korosho ili kuhamasisha ulaji unaofaa na kulinda afya za wananchi.
Vilevile, amewakumbusha wananchi kutokubali kupewa pipi au bidhaa nyingine zenye sukari nyingi badala ya fedha taslimu za chenji wanaponunua bidhaa katika maduka makubwa.
Amewataka pia wamiliki wa maduka kuhakikisha hawawalazimishi wateja kupokea bidhaa zenye sukari nyingi kama mbadala wa chenji ya manunuzi, akisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira yanayochochea uchaguzi wa vyakula na vinywaji vyenye afya.