Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YASISITIZA DHAMIRA YA KUWA MFANO UTEKELEZAJI BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: November 5th, 2026

Na Clement Robert, WAF - Dodoma

Wizara ya Afya imesisitiza dhamira yake ya kuweka historia mpya nchini kwa kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unafanikiwa na kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kote.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akizungumza na menejimenti ya wizara hiyo katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa miradi na mfumo huo wa bima.

Katika kikao hicho, Mhe. Mchengerwa ameambatana na Naibu Waziri Dkt. Florence Samizi, Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe, Naibu Katibu Mkuu Bw. Ismail Rumatila, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaatiba Bw. Emmanuel Tayari na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bruno Sunguya

"Mataifa mengi yaliyojaribu zoezi hili hayakufanikiwa, ambayo inamaanisha lazima sisi tuwe mfano. Na kwa kuwa tumeanza vizuri, lazima tufanikiwe," amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa ameelekeza utaratibu wa kutambua kaya masikini zitakazopewa kadi za msamaha ufanyike kwa umakini ili kupunguza mzigo usio wa lazima kwa NHIF.

"Anaepewa awe ni yule kweli amethibitishwa kuwa ni kaya inayostahili ili kupunguza mzigo kwa NHIF. Hiyo fedha ikibaki, itawasaidia mfuko kuendelea kuwa hai," amesema Mhe. Mchengerwa

Katika kuhakikisha malengo hayo yanatimia bila kukwama, Waziri Mchengerwa ameagiza kuundwa mara moja kwa timu maalum ya ufuatiliaji wa kila siku, ili kupokea takwimu za usajili kwa wakati na kuhakikisha uendeshaji wa mfumo huo unaleta matokeo tarajiwa kwa wananchi wote.